Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Ibada ya mazishi ya Kamanda Mwandamizi wa Hizbullah nchini Lebanon, Shahidi Haitham Ali Al-Tabatabaiy (Abu Ali), pamoja na wenzake, imefanyika leo Jumatatu katika maeneo ya Dhahiya ya Kusini mwa Beirut.
Shughuli hiyo imehudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi na viongozi mbalimbali, ambapo miili ya kamanda huyo wa muqawama na baadhi ya wapambanaji wenzake – waliouawa shahidi katika shambulio la kigaidi lililofanywa jana na utawala wa Kizayuni – ilipelekwa kwa heshima kubwa miongoni mwa makundi ya waombolezaji.
Kwa mujibu wa taarifa ya Hizbullah, Haitham Ali Al-Tabatabaiy na wenzake wanne waliuawa shahidi katika shambulio la anga la Israel lililolenga eneo la Haret Hreik katika Dhahiya ya Kusini.
Akizungumza katika mazishi hayo, Sheikh Ali Damuush alisisitiza kuwa: “Ugaidi wa kuwalenga na kuwaua makamanda hautaleta udhaifu wowote ndani ya muqawama; badala yake, unazidisha uimara na uthabiti wa azma yetu.
“Njia yetu itaendelea, na hakuna kitu kinachoweza kuvunja azma yetu”
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Hizbullah alisisitiza kuwa: “Maadui wanadhani kwamba kuwaua makamanda kutaleta hitilafu ndani ya muqawama, lakini hawajui kwamba sisi tuna makamanda jasiri, waaminifu na wenye imani thabiti ambao katu hawataonyesha udhaifu katika uongozi wala katika nia yetu.”
Akaongeza kuwa: “Mashahidi wetu walisimama imara kwa nguvu zao zote na kwa kutumia nyenzo walizokuwa nazo kukabiliana na adui, ili kulinda heshima na uhuru wa Lebanon. Njia hii itaendelea, na serikali ya Lebanon inapaswa kuweka mpango wa kuzuia kukubali masharti ya Israel na Marekani.”
Sheikh Ali Damuush, akisisitiza msimamo wa utendaji wa Hizbullah, alisema: “Kulegeza msimamo au kukubali mashinikizo ya Marekani na Israel hakutaleta matokeo yoyote. Sisi hatutasalimu amri; hata kama maadui wataweka juhudi zao zote kutuangamiza, kamwe hatutaacha muqawama wala kujitoa katika kuilinda nchi yetu.”
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Hizbullah pia aliwakumbuka kwa heshima mashahidi wa muqawama, hususan Sayyid Hassan Nasrallah, Sayyid Hashim Safiuddin, Shahidi Haitham Ali Al-Tabatabaiy, pamoja na mashahidi wengine wa njia ya Quds, akisema: “Tutaendelea kusimama pamoja na mashahidi wetu na kulinda uhuru wa Lebanon. Kwa nguvu zote tutakabiliana na Israel na maadui wa nchi. Njia hii ni yetu, na hakuna kitu kinachoweza kuivunja azma yetu.”
Beirut; Uwanja wa Umoja wa Kitaifa Dhidi ya Uvamizi wa Israel
Wakati utawala wa Kizayuni ukiendeleza uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano na kuendeleza mauaji ya wapinzani, huku serikali ya Lebanon ikionekana kushindwa kuchukua hatua dhidi ya uovu wa Israel, leo — sambamba na mazishi ya mashahidi wa shambulio la hivi karibuni — wananchi kadhaa wa Beirut waliingia mitaani katika Mtaa wa Hamra, wakitoa kauli dhidi ya ukaliaji wa mabavu na kulaani uvamizi wa Israel, huku wakisisitiza haki ya muqawama na kukataa njama za kuhalalisha uhusiano na Israel.
Katika maandamano hayo, kauli kama:
“Hakuna madhehebu yoyote ambayo iko salama mbele ya uvamizi wa Israel”
zilisikika, na waandamanaji wakaitisha kusitishwa kwa mauaji ya kila siku, kuachiliwa kwa raia wa Lebanon wanaozuiliwa, na kukomesha uharibifu unaofanywa kwa makusudi katika vijiji vya mpakani.
Wananchi waliokuwepo katika maandamano hayo walitangaza:
“Sote tutashinda pale tutakapoungana dhidi ya uvamizi wa Israel.”

Your Comment